Mtaalamu wa Qur’ani Tukufu wa nchini Kuwait asema hakuna haja ya kuongeza makundi mapya Katika Sehemu ya wanawake yamMashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Iran
Badriyah al-Abduli yupo Mashhad akihudumu kama mmoja wa majaji katika sehemu ya wanawake kwenye raundi ya fainali ya toleo la 41 la mashindano hayo.
Akizungumza na IQNA pembezoni mwa mashindano hayo, alisema kuwa makundi mawili ya sasa, ambayo ni hifdh (uhifadhi) wa Qur’ani yote na usomaji wa Tarteel, yanatosha na hakuna haja ya kuongeza makundi mengine mapya.
Kuhusu kiwango cha washiriki, alisema kuwa kwa ujumla, wanaweza kusemwa kuwa wako katika kiwango cha wastani, ingawa baadhi yao wamefanya vizuri sana.
Al-Abduli pia alisema kuwa kanuni za mashindano hayo ni nzuri na zinakubalika, huku mfumo wa tathmini ya alama ukiwa wa uwazi wa kutosha bila matatizo yoyote.
Athari za Mashindano ya Qur’ani Tukufu kwa Vijana
Alipoulizwa kuhusu jinsi mashindano ya Qur’ani yanavyoweza kuwahamasisha vijana kuhifadhi na kusoma Qur’an, alisema kuwa Qur’an Tukufu imeteremshwa kwa ajili ya waislamu wote na wanadamu kwa ujumla, wakiwemo vijana.
"Kusoma Qur’an, hasa kwa vijana, kuna faida za kiroho na athari chanya katika jamii. Kwa hivyo, ni muhimu kuwaelekeza zaidi kwenye Qur’ani kupitia programu mbalimbali, hasa mashindano ya Qur’an," alisema.
Aliongeza kuwa kukusanyika kwa wawakilishi kutoka nchi za Kiislamu katika taifa kama Iran, ambalo linabeba jina la Uislamu, na katika mazingira ya kiroho ya Haram Takatifu ya Imam Reza (AS) huko Mashhad, kunaimarisha misingi ya dini na Uislamu. Hili linaweza kuwa hatua kuelekea kuunda ustaarabu mpya wa Kiislamu unaojengwa juu ya misingi ya Qur’an.
Soma Zaidi:
Msomaji wa Qur’ani Tukufu wa Misri Asifu Uratibu wa Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Iran
Kwa kumalizia, alisema: "Nawashukuru waandaaji wa mashindano haya na natumai tutapata baraka kubwa za kiroho tukiwa karibu na Haram Takatifu ya Imam Ridha (AS).
Washiriki wa usomaji na uhifadhi wa Qur’ani kutoka nchi 144 walishiriki katika raundi za awali za Mashindano ya 41 ya Kimataifa ya Qur’an ya Iran, na kati yao, wawakilishi kutoka nchi 27 wamefika hatua ya fainali katika sehemu za wanaume na wanawake.
Fainali hizo, zinazoendelea katika mji mtakatifu wa Mashhad, zitahitimishwa siku ya Ijumaa kwa hafla ya kufunga mashindano ambapo washindi bora watazawadiwa.
Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huandaliwa kila mwaka na Shirika la Awqaf na Misaada ya Hisani la Iran.
Lengo lake ni kueneza utamaduni wa Qur’ani miongoni mwa waislamu na kuonyesha vipaji vya wasomaji na wahifadhi wa Qur’ani Tukufu.